Wananchi watakiwa kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa |
|
Serikali imewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa leo Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akihitimisha mkutano wa 16 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waziri Mkuu amewataka Wananchi kujitokeza kujiandikisha, kugombea na kupiga kura kuwachagua viongozi watakaowaongoza katika ngazi za Mitaa, Vitongoji na Vijiji katika kipindi cha miaka Mitano. Katika hotuba yake, Waziri Mkuu amewataka Wabunge na Madiwani kujitokeza kuwahamasisha Wananchi kushiriki katika uchaguzi huo ili kutekeleza takwa la Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalosema kuwa kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa. Waziri Mkuu Majaliwa pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini, kuvisimamia vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuna amani na utulivu wakati wote wa kampeni na wakati wa uchaguzi. Kwa upande wa Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa uchaguzi huo, Waziri Mkuu amewatska kuhakikisha wanasimamia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa ili ufanyike katika misingi ya uhuru na haki. |